PAZIA la Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) linafungwa leo kwa mechi tano kuchezwa kwenye viwanja mbalimbali hapa nchini na kubwa linalosubiriwa ni kuona ni timu gani itaibuka bingwa kati ya JKT Queens au Simba Queens.
JKT Queens ndiyo inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 43 na haijapoteza mchezo wowote hadi sasa na leo itacheza na Mkwawa Queens mkoani Iringa kama ilivyo kwa Simba yenye pointi 42, itakuwa mkoani humo kuikabili Ceasiaa Queens.
JKT inapewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa leo kama itaifunga Mkwawa, huku Simba ikiombea maafande hao ipate walau sare na yenyewe ishinde ili iwe bingwa.
MSIMU ULIKUWA WA MOTO
Kama kuna msimu ulikuwa moto tangu Ligi Kuu ya Wanawake ianzishwe msimu wa 2016/17, huu ni mmojawapo na hata baadhi ya makocha wamekiri hilo.
Timu nyingi zilipambana na hata zile zinazojiita vigogo licha ya kwamba zilishinda mechi zao nyingi, zilitoka jasho.
"Msimu huu ulikuwa balaa kwani ushindani ni mkubwa sana, timu karibu zote zilionyesha soka zuri na ilikuwa ni ngumu kupata ushindi kirahisi," alisema Kocha wa JKT Queens, Ali Ali.
Kocha wa Simba Queens, Charles Lukula alisema "Ligi imekuwa ngumu sana tofauti na msimu uliopita, kwani safari hii ile hali ya kwamba unazifunga timu mabao mengi mara nyingi haipo, ukiangalia Simba tumepata ushindi wa mabao saba mara mbili tu. Pia uwepo wa wachezaji wengi wa kigeni umeifanya ligi kuchangamka.
Kiungo wa Yanga Princess, Maimuna Hamis'Mynaco' alisema; "Ukitaka kujua ligi ya msimu huu ni ngumu, bingwa anapatikana mechi ya mwisho, hiyo inamaanisha wachezaji kutoka timu zote walikuwa bora sana.
VITA YA TIMU NNE USIPIME
Ligi ya msimu huu ilivyoanza wengi walizipa nafasi timu nne kuwania ubingwa ambazo ni mabingwa watetezi, Simba, Fountain Gate Princess, JKT Queens na Yanga Princess kutokana na usajili iliofanya na kuwa na wachezaji wazoefu.
Simba na Yanga zilianza msimu kwa kipigo kabla ya kukaa sawa na kufanya vizuri lakini baadae Yanga ikaja kupotea mwishoni kwenye mzunguko wa pili na kuacha vita ya timu tatu na sasa hatimaye zimebaki mbili Simba na JKT zikitafuta ubingwa leo.
"Ligi ya msimu huu iligawanyika katika makundi matatu, timu nne zinazowania ubingwa, tatu zinazowania nafasi za katikati na nyingine tatu zilizo mwishoni.
"Ceasiaa walifanya usajili mzuri lakini sijajua walikwama wapi kwani nilitarajia wangekuwa miongoni mwa timu zinaowania ubingwa lakini wakapoteana," anasema kocha wa Alliance Girl, Ezekiel Chobanka.
"Sisi kama Alliance malengo yetu tumetimiza kwani wakati ligi inaanza nilishasema kama tukipambana sana basi tutamaliza nafasi ya nne au tano.
REKODI
JKT Queens imeweka rekodi ya kuwa timu iliyoruhusu mabao machache zaidi msimu huu ikiwa imefungwa sita, kabla ya mechi yake ya mwisho leo, huku timu iliyofungwa mabao mengi zaidi ni The Tiger Queens ya Arusha iliyofungwa 49 kabla ya mechi yake ya leo dhidi ya Fountain Gate Princess.
Simba Queens imeweka rekodi ya kuwa timu iliyofunga mabao mengi zaidi kwenye ligi hiyo hadi sasa ikiwa imefunga mabao 51 kabla ya mechi yake ya mwisho leo dhidi ya Ceasiaa Queens ikifuatiwa na JKT iliyofunga mabao 39.
HAT-TRICK ZAPAMBA MOTO
Msimu uliopita hadi ligi inamalizika zilifungwa hattrick 10, lakini msimu huu zimefungwa hat-trick tisa tu.
Wachezaji Winfrida Charles wa Alliance Girls na Donisa Minja wa JKT Queens wamefunga hat-trick mbili kila mmoja wakati Jetrix Shikangwa wa Simba Queens, Blessing Nkor(Yanga Princes), Cynthuia Musungu (FountaiN Gate), Joanitha Ainembabazi( Ceasiaa) na Stumai Abdallah wa JKT Queens wakifunga hat-trick moja kila mmoja
Winfrida alifunga hat-trick katika michezo yote miwili dhidi ya Mkwawa Queens ambayo Alliance Girls ilishinda mbao 3-0 kila mchezo, huku Donisia alifunga hat-trick hizo walipoibamiza The Tiger mabao 6-0 na Mkwawa mabao 6-1.
REKODI YA ASHA YASHINDWA KUVUNJWA
Msimu uliopita straika wa Simba Queens, Asha Djafar ndiye aliibuka mfungaji bora kwa kufunga mabao 27, lakini msimu huu anayeongoza kwa ufungaji ni Jentrix Shikangwa wa Simba mwenye mabao 16, jambo linaloonyesha hawezi kuifikia rekodi hiyo.
Asha msimu huu umeonekana haukuwa mzuri kwake kwani mara nyingi alianzia benchi na hadi sasa kabla ya mechi ya mwisho leo, amefunga mabao manane, hivyo kushindwa kuifika rekodi yake mwenyewe.
MABAO MACHACHE
Ligi ya msimu huu imedhihirisha ugumu wake kwani hata idadi ya mabao ya kufunga kwa timu imepugua.
Msimu uliopita hadi ligi inamalizika mabao 470 yalifungwa kwa timu zote 12 zinazoshiriki ligi hiyo, tofauti na msimu huu hadi sasa wakati ikiwa imebaki mechi moja kwa kila timu zitakazofanyika leo ni mabao 247 tu yamefungwa kwa timu 10 zinazoshiriki.
Usajili mkubwa ambao timu nyingi zilifanya msimu huu ulichangia kuifanya ligi kuwa ngumu hivyo kupungua kwa mabao.
Pia kuondoka kwa baadhi ya mastaa kama Opah Clement anayecheza soka la kulipwa nchini Uturuki, Aisha Masaka (Sweden) pamoja na kuwa nje ya uwanja wa straika hatari wa Yanga Princess, Clara Luvanga, inatajwa kuchangia kupungua kwa mabao kwenye ligi hiyo kwani wachezaji hao ni kati ya wafungaji mahiri.
Msimu uliopita hadi ligi inamalizika Simba ilikuwa kinara wa ufungaji kwa kufunga mabao 94, wakati msimu huu hadi sasa kabla ya mechi ya leo imefunga 51, huku Fountain Gate msimu ulipita ilifunga mabao 65 lakini msimu huu mpaka sasa imefunga 35.
RATIBA LEO
Ceasiaa Queens vs Simba Queens
Alliance Girs vs Baobab Queens
Mkwawa Queens vs JKT Queens
Fountain Gate vs The Tigers Queens
Amani Queens vs Yanga Princess
Post a Comment